Saturday 10 May 2014

ATHARI ZA KUOANA NA MTU ASIYE AMINI


Pr. Lupakisyo M.Mwakasweswe
Chaplain - Chuo Kikuu Cha Arusha

Fungu kuu:  1 Wakorintho 7:39 Mwanamke hufungwa maadamu mumewe yu hai, lakini ikiwa
                      mumewe amefariki, yu huru kuolewa na mtu ye yote amtakaye; katika Bwana tu.

Utangulizi
Ndoa ni agizo la Mungu, ni mpango wa Mungu tangu mwanadamu alipoumbwa katika bustani ya edeni, haukuwa mpango wa Mungu kwamba aumbe mwanadamu ili aishi katika ulimwengu wenye shida, Dhambi ilipoingia duniani, mpango wa Mungu wa kumwuumba mwana damu awe mwenye furaha ukabadilika kwa jinsi mwanadamu mwenyewe alipo kubali kuasi sheria ya Mungu, mwanadamu aliposikiliza agizo la Shetani, ulikuwa ndiyo mwanzo wa maisha yenye huzuni.
Neno kuoa au kuolewa ni tendo la kuanzisha uhusiano kati ya mwanamke na mwanaume. Ndoa yaweza kuelezewa kwa maana nyingi lakini moja niliyo ichagua mwandishi wa Lessoni ya Dini ya Mahusiano ya July 2004 uk wa 45 alisema “ Ni muunganiko wa mwanamume na mwanamke katika njia halali “, tena mwanafalsafa Aristotle alipuliuzwa kueleza maana ya neno rafiki alisema “ Rafiki ni roho moja ikiishi katika miili miwili.” Kwa maana hizo tunaweza kujenga hoja yetu kwamba Mungu alikusudia kwamba watu wanao oana ni wale ambao wanafanya mahusiano yanayo kubalika na mbingu, tena wakiwa tayari wamejiandaa kuishi pamoja kuwa mwili mmoja. Hilo ndilo ndoa katika Bwana tu

Asili ya Ndoa
Mwanzo 18:18 – 25 Bwana Mungu akasema, Si vema huyo mtu awe peke yake, nitamfanyia msaidizi wa kufanana naye.19 Bwana Mungu akafanyiza kutoka katika ardhi kila mnyama wa msituni, na kila ndege wa angani, akamletea Adamu ili aone atawaitaje; kila kiumbe hai, jina alilokiita Adamu likawa ndilo jina lake. 20 Adamu akawapa majina yao kila mnyama wa kufugwa, na ndege wa angani, na kila mnyama wa mwituni; lakini hakuonekana wa kumsaidia Adamu aliyefanana naye. 21 Bwana Mungu akamletea Adamu usingizi mzito, naye akalala; kisha akatwaa ubavu wake mmoja, akafunika nyama mahali pake, 22 na ule ubavu alioutwaa katika Adamu Bwana Mungu akaufanya mwanamke, akamleta kwa Adamu. 23 Adamu akasema, Sasa huyu ni mfupa katika mifupa yangu, na nyama katika nyama yangu, basi ataitwa mwanamke, kwa maana ametwaliwa katika mwanamume. 24 Kwa hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja. 25 Nao walikuwa uchi wote wawili, Adamu na mkewe, wala hawakuona haya.
Maisha yenye huzuni ni pamoja na kuzaa kwa uchungu, kula kwa jasho, mahusiano yasiyo sahihi kwa wana ndoa, uchaguzi mbaya wa mwenzi nk. Katika mada hii tutazingatia athari za kuoana na mtu asiye amini.
Mungu ndiye anayejua ninani atakaye kuwa msaidizi wako, kwa hiyo usisumbuke kutafuta msaidizi yoyote mpaka Mungu amekupatia. Waweza kujiuliza anakujaje? Mungu analeta mtu kwa wakati wake, Muda ukifika na umekuwa ukimtegemea atakupatia sawa sawa na mapenzi yake.Kuna athari kubwa sana kukataa mwongozo wa Mungu katika kuchagua mwenzi wa maisha, wahenga walisema “ Majuto ni mjukuu”. 1 Wakorintho 7:39 Mwanamke hufungwa maadamu mumewe yu hai, lakini ikiwa mumewe amefariki, yu huru kuolewa na mtu ye yote amtakaye; katika Bwana tu.
 Maoni ya baadhi ya vijana kuhusu kuolewa na kuoana na Wasio amini
·         Hakuna madhara yoyote yakuoana na mtu asiye amini kwani ni mtu ninaye pendana naye sana.
·         Mtu asiye Msabato anamaendeleo kuliko msabato kwa sababu wasabato wengi hawajishughulishi.
·         Ndani ya kanisa vijana wakubwa ni wachache , wamebaki watafuta njia tu, yaani (PF)
·         Wasichana wa hapa kanisani ni wahuni sana.
·         Mbona ni mwaaminifu kuliko vijana wa kanisa letu?
·         Nina mfahamu siku nyingi hawezi kuwa na tabia mbaya kivile
·         Nimepanga kumleta kanisani tukisha oana tu, naamini ataongoka tu
·         Dini pekee haiwezi kutufikisha mbinguni, hata vijana wa kisabato wanafanya maovu mengi kuliko wasio wasabato.
·         Kijana wa kisabato mpaka akuoe basi amekuonea huruma kwamba ameshakuchezea sana (ni wachafu kitabia).
·         Kwa upande na wanaume husema kuwa wasichana walioko nje ni waaminifu kiliko wanawake wa ndani, na kwa wanaweke husema vivyo hivyo.
·         Wanaume wa kisabato huwataka wasichana kwa kuwachezea kwanza ndipo kaamuu kama watawaoa au lah!
Mwongozo wa kanisa (Kanuni za Kanisa)
Ndoa na Familia ni msingi wa 23 katika mwongozo wa kanisa la Wa adventista wa Sabato uk 190. Unasema “ Ndoa ilianzishwa na Mungu katika Edeni na kuthibitishwa na Yesu kuwa ni muungano wa maisha yote kati ya mwanamume na mwanamke katika urafiki wa upendo. Kwa mkristo ahadi ya ndoa ni kwa Mungu pia kama ilivyo kwa mwenzi, na hainabudi kutolewa kati ya watu wenye imani moja tu
Kuoa na kuolewa - Agano la kale
Kumbukumbu la torati 7:1 – 4 Bwana, Mungu wako, atakapokutia katika nchi uendayo kuimiliki, atakapoyang'oa mataifa mengi watoke mbele yako, Mhiti, na Mgirgashi, na Mwamori, na Mkanaani, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi, mataifa saba makubwa yenye nguvu kukupita wewe; 2 wakati Bwana, Mungu wako, atakapowatoa mbele yako, nawe utawapiga; wakati huo ndipo uwaondoe kabisa; usifanye agano nao, wala kuwahurumia; wala usioane nao; 3 binti yako usimpe mwanawe mume, wala usimtwalie mwanao mume binti yake. 4 Kwa kuwa atamkengeusha mwanao mume asinifuate, ili wapate kuabudu miungu mingine; ndipo itakapowaka hasira ya Bwana juu yenu, naye atakuangamiza upesi.
 Kumbukumbu laTotrati 18: 9 Utakapokwisha kuingia katika nchi akupayo Bwana, Mungu wako usijifunze kutenda kwa mfano wa machukizo ya mataifa yale.10 Asionekane kwako mtu ampitishaye mwanawe au binti yake kati ya moto, wala asionekane mtu atazamaye bao, wala mtu atazamaye nyakati mbaya, wala mwenye kubashiri, wala msihiri, 11 wala mtu alogaye kwa kupiga mafundo, wala mtu apandishaye pepo, wala mchawi, wala mtu awaombaye wafu. 12 Kwa maana mtu atendaye hayo ni chukizo kwa Bwana; kisha ni kwa sababu ya hayo Bwana, Mungu wako, anawafukuza mbele yako. 13 Uwe mkamilifu kwa Bwana, Mungu wako.
Kwa mafungu hapo juu, Mungu alipowapa nchi wana wa Israeli alitaka waishi maisha makamilifu. Mungu alifahamu uwepo wa makabila ambayo hayakumpenda Mungu kwa sababau waligeukia miungu mingine. Mungu alitahadharisha wazazi na watoto kwamba wasifanye maagano nao wala wasioane nao, maana kuna kukengeushwa.
Unapoanzisha uhusiano wa ndoa, kumbuka kwamba una mvuto mkubwa wa mahusiano ya ngono,na hi iimefanya wengi kujikuta wameingia katika tendo la ndoa kabla ya wakati wao. Kuwa na uhusianao na makabila yaliyo mwasi Mungu Mhiti, na Mgirgashi, na Mwamori, na Mkanaani, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi, mataifa saba makubwa yenye nguvu kupita Israeli Mungu alionya wasiwe na mahusiano nao kwa kuwaozesha wana wao. Endapo unafahamu mwenendo mbaya wa mtu Fulani na hujaweza kumwambia ni rahisi sana ukaiga mwenendo huo.


Kuoa na kuolewa – Agano jipya
2 Wakorintho 6:14 -18 Msifungiwe nira pamoja na wasioamini, kwa jinsi isivyo sawasawa; kwa maana pana urafiki gani kati ya haki na uasi? Tena pana shirika gani kati ya nuru na giza?15 Tena pana ulinganifu gani kati ya Kristo na Beliari? Au yeye aaminiye ana sehemu gani pamoja na yeye asiyeamini? 16 Tena pana mapatano gani kati ya hekalu la Mungu na sanamu? Kwa maana sisi tu hekalu la Mungu aliye hai; kama Mungu alivyosema, ya kwamba, Nitakaa ndani yao, na kati yao nitatembea, nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu.17 Kwa hiyo, Tokeni kati yao, Mkatengwe nao, asema Bwana, Msiguse kitu kilicho kichafu, Nami nitawakaribisha.18 Nitakuwa Baba kwenu, Nanyi mtakuwa kwangu wanangu wa kiume na wa kike.
Mtu mwingine aweza kusema, fungu hili linamaana nyingine na siyo muungano wa ndoa. Hata kama mwandishi wa fungu hili ametaja jambo lingine  ukweli unabaki pale pale kwamba mahusiano ya muumini na mtu asiye muumini haiwezekani  labda yawe  mahusiano yaliyo katika Bwana,  ndiyo yanayofaa, mahusiano yoyote yasiyo mpendeza Mungu hayangefaa kwa mtu wa Mungu, iwe ni katika kuoa au kuolewa au katika mahusiano ya kibiashara isiyo halali. Mungu anataka kutengana na watu wasiomwamini.
Wengi wametumia fungu kuhalalisha kuoana na mtu asiye amini kwa kusoma fungu la 1Wakorintho 7: 12 - 14 “Lakini watu wengine nawaambia mimi, wala si Bwana, ya kwamba iwapo ndugu mmoja ana mke asiyeamini, na mke huyo anakubali kukaa naye asimwache. 13 Na mwanamke, ambaye ana mume asiyeamini, na mume huyo anakubali kukaa naye, asimwache mumewe. 14 Kwa maana yule mume asiyeamini hutakaswa katika mkewe; na yule mke asiyeamini hutakaswa katika mumewe; kama isingekuwa hivyo, watoto wenu wangekuwa si safi; bali sasa ni watakatifu.”
 Mwandishi anafundisha  waumini waliokutwa na injili wakiwa tayari katika mahusiano ya mke na mume , hakukuwa na sababu ya kuachana ila kuonyesha upendo wa Kristo kwa mwenzi wake na ili aiamini injili. Hapa haiwezi kuwa kibali cha mtu kuoa au kuolewa na mtu asiye amini.
Ndoa ya zaidi ya Mke Mmoja
Hebu tuangalie mazingira yamtu anaye owa au kuolewa katika ndoa ya Zaidi ya mke mmoja; Kitabu cha Mwongozo wa Kanisa uk 214 tole la 18 sahihisho la 2010 unasema “Desturi ya kuwa na wake wengi miongoni mwa watu wasio Wakristo tunao wahubiria injili katika makabila mengi, hupingana na kanuni za Kikristo. Kwa hiyo Kanisa letu limeshika maelekezo yafuatayo:
1.      Mtu akiwa na wake wengi wakati injili inapomfikia, akibadilika moyo, basi atatakiwa kuitengeneza hali yake kwa kuwaacha wake zake wote na kubaki na mmoja tu, kabla hajahesabiwa kustahili ubatizo na kuingia katika ushirika wa kanisa.
2.      UK 216 namba 4 inasema “Tunatambua na kukubali haki ya mke, aliyeachwa na mume mwenye wake wengi kuolewa tena.
3.      Uk 216 namba 5 inasema “Wake za mtu walioolewa naye walipokuwa hawamjui Mungu, ambao baada ya kupokea imani ya Kikristo hawawezi kuachana na mume wao kutokana na sababu na desturi za kimila/utamaduni, wakipata kibali cha kamati ya Konferensi, au union wanawezakubatizwa na kupokelewa katika ushirika wa kanisa . Lakini mwanamke aliyemshiriki akiolewa kama mke wa pili au zaidi, ataondolewa katika ushirika wa kanisa, na hatapokelewa tena katika ushirika wa kanisa
mpaka aachane na Yule mume.
Hayo ni mazingira ya watu, wanawake na wanaume walio ndani ya ndoa na wamepata injili bada ya kuoa na kuolewa, kwa hiyo mtu asitumie mafungu ya Biblia kuficha ukweli kuhusu mahusiano ya mke na mume.
Nabii wa Mungu Ellen G. White akiandika katika kitabu cha Kutayarisha njia sehemu ya 1, uk 137.  anasema. “ Wale wanao iungama kweli huyakanyaga mapenzi ya Mungu kwa kuoana na wasioamini; wanapoteza kibali cha Mungu na kufanya kazi ngumu ya kutubu. Huenda mtu asiyeamini akawa mwenye tabia njema ya moyoni lakini kwamba hajaungama majibu ya madai ya Mungu naye amekataa wokovu mkuu namna hii ni sababu ya kutosha inayo acha umoja usikamilishwe. Pengine tabia ya Yule asiye amini ikafanana na ile ya Yule kijana ambaye Yesu alimwambia maneno haya, “Umepungukiwa na neno moja;” hilo litakuwa neno moja lenye kutakikana sana.”
Nuru kwa kanisa uk 141 Mwandishi anasema “Kamwe watu wa Mungu wasingethubutu kuingia mahali palipokatazwa na Mungu. Ndoa baina ya waaminio na wasio amini imekatazwa na Mungu. Lakini mara nyingi moyo usioongoka hufuata tama zake mwenyewe, na ndoa zisizo kubaliwa na Mungu hufanywa. Kwa sababu hii wanaume na wanawake wengi hawana tumaini wala hawanaye Mungu ulimwenguni. Mivuto yao bora imekufa kwa mnyororo wa hali ya mambo haya wameshikwa wavuni mwa shetani. Wale wanaotawaliwa na ashiki na tama mbaya ya mwili watakuwa na mavuno machungu kuvuna katika maisha haya, na mwenendo wa waweza kuleta hasara ya roho zao mwishowe.
Amosi 3:3 Je! Watu wawili waweza kutembea pamoja, wasipokuwa wamepatana?. Kwa muktadha wa Biblia, watu wawili hawawezi kutembea pamoja kama hawajapatana. Kwa watu wana mwamini Mungu hawataweza kupatana na mtu asiye mpenda Mungu , watapatana tu kwa sababu ya kuongoa roho na sio kwa sababu ya kuoa na kuolewa. Vijana wengi waetumia njia hii kuhalalisha ndoa za imani tofauti kwa kusingizia kwamba wamepatana. Mungu anataka watu wake wapatane katika mambo matakatifu.m Ndoa ni Takatifu kama ilivyo Sabato, wale wanaoingia katika muunganik wa tendo hili ni wajibu wao kuchukua tahadhali ili wasije wakajikuta wanafanya mapatano na mtu asiye muumini wa imani yake.
Nuru kwa kanisa uk 143 Mwandishi anasema “ Kila Mkristo apaswa kufanya nini akiingizwa mahali pa kujaribiwa nguvu ya imani yake?.  Kwa uthabiti wenye kustahili kuigizwa yampasa aseme dhahiri: “Mimi ni mkristo mwaminifu. Naamini kuwa siku ya saba ya juma ni Sabato ya Biblia. Imani na kanuni zetu zimeachana, ni tofauti hata hazipatani. Hatuwezi kufurahi pamoja, mana kama nikiendelea kujipatia ujuzi kamili zaidi wa mapenzi ya Mungu, nitazidi kuhitilafiana na walimwengu na kufanywa nifanane zaidi na kristo.”
Mwongozo wa Kanisa uk 170 toleo la 18 sahihisho la 2010 unasema “Kwa kawaida roho ya Unabii inashauri dhidi ya ndoa kati ya “anayeamini na asiyeamini” na inatoa tahadhari zaidi dhidi ya kuungana na Wakristo wenzetu ambao “hawajaupokea ukweli wa wakati huu”. – 5T 364.Inaendelea Kwa kusema “Kanisa linatambua kwamba ni haki ya mtu binafsi kufanya uamuzi wa mwisho kuhusu uchaguzi wa mwenzi wa ndoa. Hata hivyo, ni tumaini la Kanisa kwamba kama mshiriki atachagua mwenzi ambaye si mshiriki wa Kanisa, wenzi hao watatambua na kuelewa kuwa Mchungaji wa kanisa la Waadventista wa Sabato aliyeahidi kusimamia kanuni zilizelezwa hapo juu , hatatarajiwa kufungisha ndoa hiyo. Mshiriki akiingia katika ndoa ya aina hiyo, kanisa halina budi kuonesha upendo na kujali kwa kusudi la kuwatia moyo wanandoa hao kuingia katika umoja kamili ndani ya Kristo.
Pamoja na hayo, katika ukursa wa 210, Mwongozo wa Kanisa unasema, “Ndoa ya Kikristo– Kwa sababu tunakubali kwamba kanisa hupimwa kutokana na kawaida zake za mema na mabaya, na kwamba ndoa ya Kikristo inayokubalika na wengi inafaa kwa wakristo wa Kanisa la Waadventist wa Sabato, tunasisitiza ushauri kuwa makanisa yetu yote yawafundishe washiriki wao kupata huduma ya ndoa ya kisheria na kikanisa, ambapo watu wanaoona hupatana na kuzishika kanuni zinazotawala ndoa ya Kikristo.
Inashauriwa kwamba mshiriki akioa au kuolewa na mtu aliye katika darasa la ubatizo, apate pia huduma hiyo ya kisheria na Kikanisa. Kama watu walio katika darasa la ubatizo wameoana kwa njia ya kimila, basi inashauriwa wafanyiwe huduma ya kisheria na ya Kikanisa kabla hawajabatizwa.
Adventist Home, uk 61 – 69 Mwandishi anasema “Ni jambo la Hatari kufanya ndoa ya kidunia. Shetani ajua Sana kuwa saa ya ndoa ya vijana wa kiume na wa kike hufunga historia ya maisha yao ya dini na ya manufaa. Hawamo kwa kristo. Pengine kwa muda mfupi watafanya jitihada kuishi maisha ya kikristo; lakini jitihada zao zote zinakutana na mvuto wa nguvu unazipinga.”


Miongoni mwa Athari za kuoana na Mtu asiye amini
Athari za kuoana na mtu asiye amini kama zinavyo andikwa na Mjumbe wa Mungu Ellen G. White katika kitabu cha Kutayarisha Njia 1 uk 137.  Anasema;
1.      Kupungua kwa hali ya mambo ya kiroho huanzia dakika ile ya kuahidi kwa kiapo kwenye mimbara
2.      Moyo wa bidii wa mambo ya dini unapunguzwa, na ngome moja mja huvunjwa mpaka wote wote wawili wamekuwa hali moja chini ya bendera nyeusi ys shetani.
3.      Katika furaha ya Harusi roho ya kidunia hushinda dhamiri, imani na kweli
4.      Katika nyumba hiyo mpya na saa ya maombi haiheshimiwi tena. Wamejichagua wenyewe na kumfukuzia mbali Yesu.
5.      Furaha anasa za kidunia hupendelewa sasa ili kumfurahisha mwenzi mpagani.
6.      Mwenzi hatapenda kusoma ama kusikiliza Biblia kisha atasema: “Ulioana na mimi, ukijua kwamba nalikuwa hali hii nilivyo sasa; sitaki kusumbuliwa”
7.      Kisha mashaka hujongea taratibu juu ya mambo ya Mungu na hatimaye anapoteza imani
8.      Uchaguzi unafanyika sasa aidha apote upendo kwa Mungu kabisa kisha adumishe upendo wa mwenzi wake asiyeamini ama aupoteze kwa mwenzi kisha ndoa ipasuke.

4 comments:

Unknown said...

nimeipenda sana hii...barikiwa sana mtu wwa Mungu!!

Unknown said...

Barikiwa

Unknown said...

Ubarikiwe sana Mchungaji,Endelea kuzijenga ndoa zetu na kuwaa daa vema vijana wetu.

Unknown said...

Mungu akubariki sana pasta endelea kutubari sisi vijana

Post a Comment